sehemu ya pili

Ilipoishia…

Basi aliniruhusu nami nikamuachia nyumba na kuanza safari yangu, nilitazama akiba niliyokuwa nayo mfuko niliona kuwa nina fedha taslimu Shilingi laki sita niliamini kuwa hizi zingeweza kunifikisha mjini Dar es salaam bila shida yoyote.

Nilitembea hadi stendi ya mabasi yatokayo kwetu Bumbuta kuelekea Dar es salaam nilipata siti nikaketi na kusubiri safari ianze.

Haikuwa mara yangu ya kwanza kusafiri kwenda mjini Dar es salaam tayari nilishawahi kwenda mara kadhaa ila safari ya siku ile ilikuwa tofauti sana na zote za awali.

Abiria wengi walionekana wakiwa na furaha katika nyuso zao, ila moyoni mwangu nilijawa na mawazo na uchungu tele, sikuhisi kama ningefurahia safari hile.

Kondakta wa basi alitangaza kuwa tutachelewa kufika mjini Dar kwani gari imebadilisha barabara ya kupita baada ya daraja la Mkange kuharibiwa kwa mvua hivyo tulipita barabara mpya ambayo ilichongwa kwa dharura, kondakta alitutangazia kuwa foleni itakuwa kubwa mno hivyo alituomba kuwa wavumilivu safarini.

Pembeni yangu alikaa mkaka mmoja aliyeonekana mtanashati hasa kwa jinsi alivyovaa, alikuwa kijana ambaye kwa makadirio angeweza kuwa na umri wa miaka 24 hivi, ambayo ni sawa na mimi tu, mara zote nilimwona akiwa anaongea na simu huku akiwa anacheka kwa furaha.

Nilitamani amalize kuongea ili nimsalimu kwani tangu safari ianze sikuongea na mtu yeyote, nilimtazama kwa makini kaka yule ngozi yake nyeusi yenye kuvutia ilinifanya nisiishiwe hamu kumtazama.

Nilijisemea moyoni mwangu kaka huyu ni mrefu sana!, anaweza akawa mrefu kuliko wote ndani ya basi haha!! kisha nikatabasamu mwenyewe. Tabasamu langu aliliona na likamshtua, hapo ndipo akaacha kuongea na simu kisha akaniangalia na kuniambia.

“Samahani dada habari yako?”  alisema huku akiwa ameachia tabasamu lake.

“Nzuri tu sijui wewe unasemaje?”  nilimjibu huku nikimuangalia usoni..

“Kwangu ni salama tu, naitwa James ila wengi hupendelea kuniita Jimmy…..” aliniambia jina lake huku uso wake ukionesha furaha aliyonayo.

Binafsi nilitambua kwanini kijana Yule aliamua kunitajia jina lake kabla ya kumuuliza, basi bila hata kuchelewa nami nikamuambia jina langu “Naitwa Suzana Herman” hapo ukawa mwanzo wa urafiki wetu.

Zikapita takribani dakika ishirini bila ya kuongea jambo lolote, kichwani  mwangu nilikuwa nawaza mambo mengi ikiwemo mwenendo wa kibarua changu cha kuuza mgahawa jijini Dar, nilikuwa natamani niwahi kufika mapema ili nikutane na wasichana ambao nilikuwa nafanya nao kazi kule.

“Suzana….. unaonekana kama mtu aliyetawaliwa na mawazo sana…. Kulikoniii..?”

Swali la Jimmy lilitawanya mawazo yangu kwa wakati ule, nikamgeukia kisha nikatoa tabasamu la uongo kisha nikamjibu swali lake.

“Hapana Jimmy kawaida tu,.. kila mwanadamu huwaza si unajua…”

“Najuaaaaa…. Ila…” Jimmy alijibu kwa kubabaika kidogo, kabla hajamaliza sentensi yake nikaikatiza

“Jimmy wewe pia unaonekana mwenye furaha sana… haha! nini hiko kinakufanya uwe na furaha hivyo..?” niliuliza.

Jimmy alianza kunieleza kwanini alikuwa na furaha vile, aliniambia ni kwasababu ni mara yake ya kwanza kwenda Dar, nikamuangalia kwa umakini kama vile sikumuelewa….. nilimtaka arudie.

“Yeah…  yah  Suzana ni mara yangu ya kwanza, kutoka Dom kuingia Dar kupambana na maisha nisije kufa njaa!  Jimmy alisema huku akiniangalia.

“aaaah Jimmy…” nilishangazwa na jinsi alivyoniambia kwa vina aliendelea kunieleza zaidi.

“Kiukweli sikujui nakokwenda, nimesikia sifa za jiji na wengi wanalipenda wacha n’kapambane” Jimmy aliongea kisha alimalizia kwa tabasamu.

Moyo wangu ukaanza kumuangalia Jimmy katika sura nyingine mpya kabisaa nilishangazwa na uwezo wake wa kuunganisha maneno vizuri vile, nilimuuliza kama yeye ni mwimbaji akaniambia ndio ila hakuwahi kurekodi nyimbo yoyote, hapo nilianza kutambua kwanini Jimmy aliamua kwenda Dar hata kama hana ndugu.

Ilibidi nimueleze tu kuwa mimi haikuwa  mara yangu ya kwanza kwenda jiji Dar, tayari nilishawahi kwenda huko mara kadhaa na nina biashara zangu huko, nauza chakula kama Mama N’tilie pia najishughulisha na mambo mengine mengi tu ya akina dada.

Wakati ule akili yangu ilitengeneza maswali mengi kwa haraka, nilitamani  kumuuliza Jimmy mambo mengi sana ikiwemo wapi anakwenda kufikia, shughuli gani atakwenda kufanya huko Dar mpaka kufikia malengo yake, nilisita kufanya hivyo kwa kuhofia nisije nikamkwaza kwani ndiyo kwanza tumekutana ndani ya basi.

Baada ya safari ndefu kiasi, basi lilisimama hotelini kondakta alitangaza abiria ambao wangependa kwenda kupata chakula cha mchana wanaweza kwenda kwa dakika kumi, wakati huo nilitazama saa yangu ya mkononi na kuona kuwa ilishatimu saa nane na nusu mchana.

Jimmy aliniomba kama sitojali niende kula chakula pamoja nae, nami nilikubali kwani tayari sikuwa na mtu yoyote wa kunifariji safarini isipokuwa yeye… Nikiwa nashuka garini nilikumbuka usemi ambao wengi huusema “mara nyingi mwanamke hutafuta pumziko, mahali ambapo atajisikia kuwa yu salama”  hakika katika safari yangu nilijisikia salama kukaa na Jimmy, ingawa hatukujuana kwa muda mrefu lakini nilitamani awe pumziko langu, anitoe katika dimbwi la mawazo yaliyonikabiri kwa wakati ule.

Tulifika hotelini pale kisha tukaketi, muhudumu alikuja kutusikiliza Jimmy aliagiza chakula kisha akaniambia nami niagize chakula changu, nilianza kusita sita sikuelewa kuwa anamaanisha atanilipia au ni kwa gharama yangu mwenyewe, Jimmy aligundua hilo akasogeza kiti chake karibu yangu na kuninong’oneza “usiogope Suzana umeshakuwa rafiki yangu sasa, nitakilipia mimi”.

Nilitabasamu kisha nikaagiza chakula, haikuchukua muda mrefu chakula kililetwa mezani na tukaanza kula, nafsi yangu ilikuwa inasikia aibu kidogo hasa nilipomuona Jimmy akiniangalia kwa jicho la wizi wizi.

                             **********************************************************

Mchana ule kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Black heart alikuwa amekaa nje ya nyumba yao alionekana akiwa na mawazo mno paji la uso lilijikunja kwa hasira na chuki kwa mambo ambayo alikuwa akiyafanya.

Muda wote allijilaumu kwanini ameangukia katika mkumbo wa kufanya kazi ile, taswira ya uzuri wake tayari ilishaanza kupotea kwa kazi ya kukesha misituni usiku kucha na kukosa usingizi, mwili wake ulianza kujengeka kama vile ni mpambanaji wa mieleka kwa kazi ngumu aliyokuwa akiifanya sura yake ukiiangalia usingeweza kuamini kama ni kijana wa miaka 25 tu.

“natamani kuacha kazi hii, ah… nitawezaje kupata pesa nyingi kiasi hiki endapo nitaacha?” Black heart alikuwa akijiuliza mwenyewe nafsini mwake. Alinyanyuka alipokuwa ameketi na kuingia ndani alielekea kabati lake la kuficha vitu vyake vya siri, alifungua sanduku la chini kabisa kisha akatoa maburungutu ya fedha.

Alianza kucheka huku machozi yakimtoka nafsi yake ilikuwa ikimuuma sana akikumbuka jinsi anavyopata pesa zile… aliamua kurudisha fedha zile kisha akafunga sanduku lake na kujitupa kitandani.

Haukupita muda mrefu kabla usingizi haujampaa alisikia mlango wa geti lake ukigongwa kwa nguvu sana, aliamka na kwenda kuangalia nani alikuwa akigonga mlango.

Alipofika mlangoni alimkuta rafiki yake aliyeitwa Faraji, ndiye ambaye alikuwa akigonga mlango kwa nguvu hivyo alimkaribisha ndani lakini Faraji alikataa kisha akamuarifu Black heart kuwa muda wa kazi umewadia hivyo amekuja kumpitia waende kazini.

Black heart alirudi ndani akafungua sanduku lake la kuhifadhia vifaa vya kazi akatoa silaha za kazi, bastola moja, bunduki moja na makasha ya risasi kisha akavitia kwenye begi kubwa ambalo mara zote hulibeba mgongoni kisha alitoka nje.

“Jemedari wangu twende mzigoni….!” Aliongea Black heart huku akionesha kuwa tayari ameshavaa sura ya kazi.

Faraji ambaye kwa wakati huo alikuwa amevalia nguo nadhifu zilizoubana sawasawa mwili wake huku mgongoni mwake akiwa amebeba begi lenye vifaa vyake vya kazi, hakika ungemuona ungelisema ni Jemedari wa vita labda, au askari wa umoja wa mataifa anayepambana vita nchini Afghanistan.

Waliingia kwenye gari moja la kifahari aina ya Toyota Avensis Wagon nyeusi na kutimua vumbi kuelekea msituni mahali iliko Ngome yao, wakiwa barabarani waliongea mambo mengi sana lakini katu Black heart hakuwahi kumweleza Faraji juu ya mpango wake wa kutaka kuacha kazi ile.     

                     ********************************************************

Baada ya kumaliza kula chakula cha mchana niilinyanyuka na Jimmy na kuelekea kwenye basi tayari kwa kuendelea na safari ya Dar es  salaam tukiwa tunatembea nilimshukuru Jimmy kwa kuninunulia chakula kisha nikamwambia hakika hoteli hii wanapika chakula kizuri sana, Jimmy alicheka kidogo kisha akanambia inabidi uwe unakuja kula hapo hata ukiwa unarudi kutoka Dar.

Niligeuka nyuma na kusoma jina la hoteli ile White Butterfly Hotel ndilo jina lililokuwa linatambulisha hoteli ile, Jimmy alikuwa wa kwanza kuingia ndani ya basi kisha akaketi nami nikafuata baada yake.

“mmh.. hakika Suzana ni msichana aliyeumbika mno ebu ona jinsi anavyotembea kwa maringo..” Jimmy alijisemea moyoni mwake huku akiendelea kuchunguza uzuri aliojaliwa Suzana alimuangalia kuanzia usoni mpaka miguuni kisha akatabasamu….

Nilimuona Jimmy akitabasamu lakini sikufahamu kipi kilifana moyoni mwake mpaka kikamfanya atabasamu vile, nilifika kwenye siti nikaketi na kumshukuru Mungu kwa muda wote alionilinda katika safari.

Nilipofumbua macho niliona abiria mpya akiingia kwenye basi, alikuwa amebeba begi kubwa mgongoni, lenye rangi nyeusi kama sura yake, alikuwa amevalia suti zilizompendeza vizuri sana alikuja na kuketi siti ya jirani upande wangu wa kulia.

Moyoni mwangu nilijiuliza kuwa pale palikuwa na mtu ambaye aliketi mwanzo wa safari, lakini sasa sikumuona tena akirudi ndani  ya basi sikutaka kuchunguza sana kwani niliona ni kama mambo yasiyonihusu kufuatilia japo makonda huwa wanaagiza  kuangalia kama jirani yake amerudi ndani ya basi au la!.

Safari ilipoanza tena niliufungua mkoba wangu wa mkononi na kuangalia kama kisanduku alichonikabidhi mama yangu kipo salama, nilifurahi baada ya kukiona kipo salama kwani nilamini kuwa kilichomo ndani kingeweza kunijulisha yale yote ambayo mama yangu alikuwa akinificha kila mara nilipomuuliza, hivyo ilinipasa kukitunza vyema.

Kondakta alitukumbusha abiria wote kufunga mkanda ili kujikinga abiria wote tulifanya hivyo, nilimuangalia yule mbaba ambaye alikuwa abiria aliyepandia gari kutoka pale hotelini, naye alikuwa akifunga mkanda.

Baada ya muda nilimuona akipiga simu “Juba nimeanza safari sasa” ndiyo sauti aliyoitoa kisha akakata simu, kwa jinsi alivyoongea nikahisi labda ni mpelelezi.

Nikamrudia Jimmy ambaye wakati wote alikuwa na simu yake ya mkononi akisikiliza baadhi ya nyimbo ambazo alikuwa akijirekodi mwenyewe katika simu yake,  tulianza kuongea safari hii nilimuomba Jimmy aniimbie moja kati ya nyimbo zake nami nimsikie.

Hakuwa na hiyana Jimmy aliimba kwa sauti nzuri nami nikavutiwa na uimbaji wake, urafiki kati yetu uliendelea kukua ndani ya basi, Nilianza kuhisi moyo wangu unaganda, barafu la furaha taratibu Jimmy alizidisha ukaribu wake kwangu ambao uliibua furaha ndani ya moyo wangu, na hicho ndicho kitu nilichohitaji kwa wakati ule.

Baada ya masaa mawili ya safari ghafla wingu zito likatanda angani na mvua ikaanza kunyesha, nilianza kuhisi baridi mwilini mwangu abiria wengi walianza kutoa makoti mazito na kuyavaa madirisha waliyafunga ili kuzuia maji kuingia ndani.

Nami nikatoa kikoti changu kidogo nilichotoka nacho kijijini kwetu nikakivaa, Jimmy akatoa koti kubwa sana na kulivaa safari iliendelea tayari ilishatimu saa kumi na nusu.

Ijapokuwa nilivaa koti lakini bado nilikuwa nahisi baridi na nilikuwa natetemeka taratibu, Jimmy aligundua hili hakusema jambo lolote akavua koti lake kisha akafunika mimi, hapo nilihisi joto lisilo kifani akilini mwangu niiljiuliza kwanini Jimmy afanye vile kwani yeye hakuhisi baridi?

Baada ya dakika tano wote tulikuwa kimya nilimuona Jimmy akiwa anatetemeka kwa baridi, nilimuonea huruma nilitamani nirudishe kote kwake lakini nilifikiri angejihisi vibaya basi niliamua la kufanya huku moyoni mwangu nikajisemea liwalo na liwe.

Nikamsogelea Jimmy zaidi nikamuangalia usoni kisha nikamuambia “samahani Jimmy….!” Kabla hajauliza samahani ya nini nikamkumbatia vizuri kama vile ni mpenzi wangu kisha nikajifunika koti lake pamoja naye.

Baada ya dakika kadhaa Jimmy aliacha kutetemeka kwa baridi hapo nikajua tu kuwa tayari joto langu limemuingia vizuri kama nilivyokusudia, sasa nilimuona Jimmy akipata wasaa wa kunitazama kwa ukaribu sana, nikatambua ananiangalia kwa kunichunguza zaidi kwani jicho lake la mkato mkato lilionyesha hivyo.

Ghafla nilihisi kitu kikipita kiunoni kwangu, na kunibinya sana nilitulia tulii na kusikilizia nini hiko kingekuwa nilitambua kuwa ni mikono ya Jimmy…

“Jimmy amenishika… mmh!! Mungu wangu nisaidie…!!” Nilijisemea moyoni mwangu mapigo ya moyo wangu yalianza kwenda mbio sekunde chache nilianza kuhisi joto la mikono ya Jimmy kiunoni kwangu, sikuwa na la kufanya zaidi ya kuomba tu mvua inyamaze ili nijitoe mikononi mwake.

Jimmy alinivuta zaidi karibu na kifuani pake, nikalaza kichwa changu kifuani pake taratibu nikaanza kuhesabu mapigo ya moyo wake sikujua nini ilikuwa dhamira yake!!…

Safari ilendelea, ilipofika majira ya saa moja hivi mvua ikaacha kunyesha na hapo tayari nilitambua kuwa tumeshapita maeneo ya Magubike, Morogorona sasa tumeanza kukanyaga ardhi ambapo ni msitu tupu bado hakuna watu waliokuwa wakiishi maeneo hayo.

Foleni ya magari ilikuwa kubwa kana vile ambavyo konda wetu alituambia hapo awali, hata hivyo dereva wetu alikuwa na ujanja ambao haukutubakiza nyuma nyuma.

Abiria wote walikua kimya wengi walikuwa wameshalala kutokana na uchovu hata Jimmy anye alikuwa amepitiwa na usingizi tayari, binafsi sikupata hata lepe la usingizi kwani kichwani mwangu nilikuwa nawaza mambo mengi mno.

Nilipogeuka upande wa pili nilimuona abiria yule ambaye alipanda basi akitokea hotelini akitoa simu mfukoni na kisha akapiga… nilimsikia akisema “wataarifu Jemedari na Black Heart kuwa imebaki robo saa tu kuwasiri check point” kisha akakata simu.

Moyo wangu ulipiga Pah!!… nilishtuka kuyasikia maneno ya namna hile nilianza kujiuliza mwenyewe “Jemedari”, “Black Heart”, “robo saa kufika kwenye check point” nikajisemea moyoni huenda nimesikia vibaya…

Nilipomuangalia tena yule m’baba nilianza kuamini niliyoyasikia, nilipogeuka nyuma yangu nilimuona abiria mwenzangu ambaye alikaa karibu nami naye akiwa ametoa macho amepigwa na butwaa!! Kwa kile alichokisikia… niliamini kuwa naye alisikia maneno yale kwani muda wote alikuwa akimuangalia yule m’baba.

Nilijiuliza mwenyewe “mbona bado kama masaa mawili mpaka kufika Dar halafu huyu anasema bado robo saa mmh…!!!” nilitamani kumwamsha Jimmy nimuambie kile nilichokiskia na kuhisi moyoni mwangu nilighairi na kujipa imani kuwa kila kitu kingekuwa sawa. Labda tu ni mahali ambapo alipanga kushukia.

Itaendelea…

Tunakuomba ujiunge nasi Ili kuweza kupata hadithi nyingi zaidi mara tu zitakapochapishwa